Bima ya Mali

Kuwa mteja anayefahamu vyema huduma za Bima

Brosha hii imekusudiwa kukupa mawaidha muhimu kuhusu bima. Kama mnunuzi wa bima, unafaa kuelewa mawaidha haya ili uweze kufaidika na bima yako na pia kuepukana na changamoto yanayotokana  na kukosa maelezo sahihi kuhusu bima. Brosha hii inadokeza baadhi ya maswala unayofaa kutilia maanani kabla ya kununua bima. Brosha hii imechapishwa na Halmashauri ya Kudhibiti Bima (IRA).

Umuhimu wa Bima

Ni bayana kwamba hasara na misiba hutokea mara kwa mara maishani mwetu. Hasara na misiba hutuathiri sisi binafsi, jamii ama kuharibu mali na biashara zetu. Bima inaongozwa na busara kwamba ni wachache tu kati ya wanunuzi wengi wa bima wanaopata hasara kila uchao. Hasara na misiba hufanya waathiriwa kusononeka, kunyanyapaa, kuhangaika na pia kutamauka. Kwa hivyo, hazina iliyochangiwa na wanunuzi wengi wa bima hutumika kuwafidia wachache watakaoathirika kufuatia matukio mbali mbali. Ukweli ni kwamba, ni magari machache tu kati ya magari mengi nchini yatakayohusika kwenye ajali. Pia,  ni nyumba chache tu ambazo huteketea, ama ni watu wachache tu kati ya idadi ya wakenya wanaofariki kila mwaka.

Je, Unahitaji Bima Maishani Mwako?

Kwa hakika, unahitaji bima ili kujilinda dhidi ya matukio na misiba mbalimbali ambayo hutokea mara kwa mara. Visa kama uwizi, moto, ajali za barabarani, magonjwa na vifo vya ghafla vinapotukia, waathiriwa huenda wasiwe tayari kugharamia hasara zinazotokana na matukio haya. Kwa hivyo, wanaokosa kujipanga kwa matukio kama haya kwa kununua bima hulazimika kuitisha harambee au kukopa pesa kutoka kwa jamaa, marafiki au benki ili kugharamia hasara zinazotokea. Watu wengu huenda wakakosa uwezo wa kukopa fedha mara tu tukio litakapotokea. Mambo yanapozid, mali ya thamani ya waathiriwa kama vile shamba, gari, mifugo au vyombo muhimu vya nyumbani huuzwa ili kusimamia gharama hizo. Mara kwa mara, mali hizi huuzwa kwa njia za hasara kufuatia hali ya dharura. Mwito wa bima ni kuwa, ni muhimu kila mmoja wetu ajipange mapema dhidi ya matukio na hasara.

Aina za bima

Kuna aina mbili za bima.

Bima ya Maisha

Katika bima ya maisha, mnunuzi hulipa kiwango fulani cha pesa kila uchao ili kujihami kwa yatakayotokea maishani mwake na kuacha jamaa zake katika hali ya kusononeka, kunyanyapaa, kuhangaika na kutamauka. Malipo haya husimamia kufidiwa kwa jamii ya mnunuzi bima atakapoaga dunia. Pia, mnunuzi anaweza kupanga bima itakayomfaidi akiwa angali hai. Bima kama hii huchukuwa muda mfupi kama vile miaka mitano, kumi au ishirini pekee. Mnunuzi anaweza kununua bima kwa maisha ya mwingine kama vile kusimamia karo ya elimu ya mtoto, kwa maisha ya bibi au bwana au mwanabiashara mwenza.

Bima ya Mali

Bima ya mali au bima la jukumu (liability). Binadamu humiliki mali mbali mbali kama vile Ndege, Meli, Nyumba, Gari, Mali ya nyumbani na mengineyo. Mali hizi huhusika kwenye hasara ama kuibwa. Majanga kama vile moto, wizi, mafuriko ama ajali mbali mbali husababisha hasara kubwa kwa wamiliki mali. Baada ya hasara kuibuka, ni muhimu kwa mmiliki mali kufidiwa ili kumwezesha kuendelea na maisha yake kana kwamba hakuna hasara ilikuwa imetokea. Pia, sisi kama binadamu, tuna jukumu ya kulinda maslahi ya wenzetu tunapohusika katika harakati mbali mbali za kujikimu kimaisha. Matukio mengi  husababishwa na miradi kama vile ujenzi wa barabara, ujenzi wa nyumba za ghorofa, kuchimbwa kwa migodi au mafuta, na kadhalika. Miradi hii inaweza kusababisha hasara kwa wenzetu, kuleta majeraha, ulemavu, kifo au kuharibu mali yao na kisha kusababisha madai dhidi yetu.

Manufaa ya Bima

Utulivu na Matumaini

Ukiwa na bima, utakuwa na utulivu na matumaini kwa kuwa utakapojipata kwenye hasara, majeraha, kilema au kifo, una hakika kuwa wewe binafsi au jamaa yako watanufaika na fidia kutoka kwa kampuni ya bima. Hivyo basi, bima hujasirisha na kuondoa wasiwasi inayohusiana na mahangaiko yananayofuatia hasara.

Kuweka Akiba

Bima ni mojawapo ya njia za kuweka hazina za polepole. Bima ni aina ya akiba ya maisha. Tofauti ya akiba ya bima na akiba zingine ni kwamba, haukubaliwi kutoa akiba za bima kabla muda wa bima haujawadia ama tukio kutokea. Bima ya maisha huchochea wanunuzi wawe na mazoea ya kuweka akiba kwa muda mrefu ili kusaidia katika siku za usoni au kuwekeza biashara.

Kudhamini Mikopo

Cheti cha bima ya maisha kinaweza kutumika kumdhamini mnunuzi atakaponuia kuchukua mkopo kutoka kwa benki au kampuni ya bima ama kudhamini mtu kortini kama dhamana. Cheti cha bima ya maisha ni sawia na title deed au log book.

Kutekeleza Malengo Mbali Mbali Maishani

Binadamu wote huwa na ndoto za kufikia maishani mwao kama vile kujenga nyuma ya kifahari, kununua gari, kugharamia karo za mtoto katika shule na kadhalika. Unaweza kutumia bima ya maisha kutekeleza ndoto kama hizi.

Msamaha wa kodi

Serikali ya Kenya inakubali afueni ya kodi ya asilimia 15 kwa kila malipo ya bima (premium) hadi kiwango cha juu cha shilingi 5,000/=. Afueni hii hutolewa kwenye bima za maisha pekee. Hii ni njia moja ya Serikali ya Kenya kuwavutia watu wengi zaidi kununua bima ya maisha.

Kabla ya kuchukua bima

Kabla ya kununua bima, hakikisha yafuatayo:

 •      Ili uchukuwe bima, lazima ukusudie hatari ya upotevu wa mali kufuatia matukio mbalimbali. Mfano ni kama mwendeshaji ndege au magari ya safari rally, anayehusika na ujenzi wa barabara au mchimba migodi na kadhalika.
 •      Ikiwa shuguli zako zinawezaletea wenzako hasara basi unafaa kununua bima ya jukumu (liability insurance). Bima ya jukumu sana sana husaidia kufuatia kusababisha hasara kwa wengine kama magari ya kubeba abiria kuanguka  na kuua ama kuwajeruhi wapita njia ama kuharibu gari au mali ya wengine.
 • Watu hununua bima ya maisha kufuatia wasiwasi kuwa wakipoteza maisha yao kighafla, wanaowategemea watafidiwa ili kuanzisha maisha upya.

Tathmini hasara inayoweza kutokea kufuatia sababu inayokusababisha kununua bima. Ikiwa unaweza kusimamia hasara hizo kibinafsi, basi usinunue bima na kama hauwezi, basi nunua bima.

Uaminifu katika Mkataba wa Bima

Bima ni mkataba baina yako na kampuni ya bima. Katika kila mkataba, kuna jukumu na haki kwako mnunuzi na pia kwa kampuni ya bima. Ni sharti utilie manani mkataba huo vilivyo ili bima iweze kukuhudumia bila tatizo. Pia, ni jukumu la kampuni ya bima kutilia maanani mkataba huo. Ili uweze kutimiza jukumu lako katika mkataba wa bima, ni sharti usome na uelewe maelezo kamili ya mkataba huo. Usipoelewa jambo fulani, basi pokea maelezo zaidi kutoka kwa ajenti, dalali au kampuni ya bima. Ikishindikana basi pata ufafanuzi zaidi kutoka kwa IRA kabla hujatia sahihi mkataba huo. Ni sharti ulipe ada za bima kulingana na maagano ya mkataba.

Hati ya Bima

Mkataba wa bima na masharti yote pamoja na maelezo kabambe yako katika hati ya bima (policy). Hakikisha umepokea hati ya bima (policy) punde tu unapokamilisha kununua bima. Weka hati ya bima salama baada ya kukisoma na kukielewa. Hati ikipotea, tafadhali piga ripoti mara moja kwa polisi na uifahamishe kampuni ya bima.

Mambo ya kuzingatia unapojaza madai ya fidiwa

Watu hununua bima ili wapate kufidiwa wanapopata hasara. Mara kwa mara walalamishi hupitia changamoto kuhusu mchakato wa kuwasilisha madai ya fidai kwa kampuni za bima.

IRA ingependa kuwashuri wanunuzi bima kuzingatia maelezo yafuatayo ili kuwasilisha madai:

 1. Piga ripoti kuhusu tukio au hasara kwa kampuni ya bima, ajenti au dalali wa bima bila kuchelewa.
 2. Toa maelezo yote muhimu kwa kampuni ya bima na pia nakala za nyaraka zinazohusiana na madai hayo.
 3. Toa maelezo ya kweli kwa kujaza fomu ya madai utakayopewa na kampuni ya bima.
 4. Ikiwa tukio hilo linahusiana na wizi, ghasia ama ajali, piga ripoti kwa polisi na ushirikiane nao katika kupeleleza na kuwashtaki wahusika.
 5. Shirikiana na kampuni ya bima katika kukagua athari za hasara hiyo.

Iwapo uamuzi unaofikiwa na kampuni yako ya bima kuhusu madai au malalamiko yako hauiakuridhisha basi unaweza kuwasilisha malalamishi yako kwa IRA ukitumia anwani zilizoorodheshwa nyuma ya brosha hii. Kila mara unapotoa malalamiko yako kwa IRA, nukuu maelezo kamili ya bima yako ikiwa ni pamoja na kampuni ya bima husika, maelezo kuhusu malalamishi yako na pia nakala za nyaraka ulizonazo kuhusu malalamiko yako.

Vidokezo kuhusu bima

 1. Usinunue bima zaidi ya uwezo wako wa kifedha.
 • Nunua bima tu kwa wauzaji bima walioidhinishwa na IRA.
 • Pata ushauri kuhusu bima kutoka kwa kampuni iliyoidhinishwa kutoa bima, maajenti, mabroka au kutoka kwa IRA.
 • Ni muhimu ulipe ada za bima kikamilifu.
 • Hakikisha kwamba umenunua bima ya lazima kama vile bima ya gari.
 • Linda maslahi ya jamii yako kwa kununua bima ya maisha.
 • Linda mali yako muhimu kama vile gari, nyumba, biashara na kadhalika kwa kuyanunulia bima.
 • Nunua bima yako ya maisha mapema ili ulipe ada ndogo badala ya kulipa ada ya juu ukiinunua ukiwa mzee.
 1. Ni muhimu kununua bima ya matibabu na ajali.
 • Chukua bima ya kukuwezesha kujikimu maishani utakapostaafu.

Halmashauri ya Kudhibiti Bima (IRA)

IRA ilibuniwa na serikali mnamo mwaka wa 2006 kwa jukumu la kuweka maangalizi, kudhibiti sekta ya bima, kusimamia na pia kuhakikisha kwamba yeyote anayehusika na biashara za bima anatekeleza kazi yake kwa njia za usawa na pia kutilia maanani manufaa ya wanunuzi bima. Jukumu kuu la IRA ni kuwalinda wanunuzi wa bima na jamii kwa jumla. Nia ya IRA ni kuhakikisha kuwa wanunuzi hao wanapata huduma wanazolipia. IRA si kampuni ya bima  na hivyo haiuzi bima. IRA inawajibika kuhakikisha kuwa kampuni za bima zinashughulikia ipasavyo malalamishi yanayohusiana na bidhaa wanazouza. IRA huhakikisha kwamba ni malalamishi ya kweli pekee yanayoshughulikiwa bila kucheleweshwa. IRA pia inawajibika kuhakikisha kuwa wanunuzi bima wananunua kwenye kampuni zilizoidhinishwa na IRA wakiwemo maajenti na mabroka.

Huduma za IRA katika kusimamia maslahi ya Wakenya katika sekta ya bima ni za bila malipo. Unaweza kuelekeza suala lolote linalohusu bima kwa IRA ukitumia njia za mawasiliano zilizoorodheshwa nyuma ya brosha hii. 

S.L.P. 43505 – 00100 NAIROBI

Zep- Re Place Off Mara Road – Upper Hill, Nairobi

Simu:(254)- 020- 4996000, 0727 563110

Simu bila malipo – 0800724499

Kipepesi: (254)- 020 – 2710126

Baruapepe: commins@ira.go.ke

Tovuti: www.ira.go.ke

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *