Bima ya Mimea na Mifugo

BIMA YA MIMEA NA MIFUGO

Kilimo na uchumi

Kilimo cha mimea na ufugaji ni uti wa mgongo wa uchumi wa Kenya. Kilimo cha mazao na ufugaji kwa pamoja huipa Kenya mapato mengi kutokana na mauzo katika nchi za nje. Sekta hii ni muhimu katika kuihakikisha nchi hii  chakula cha kutosha. Sekta hizi mbili huchangia 22% ya Uchumi wa Kenya (GDP).

Matatizo yanayowakabili wakulima nchini Kenya

Kilimo cha mazao na ufugaji nchini Kenya kinakabiliwa na changamoto nyingi. Hali hii inafanya ngumu kwa wakulima wa Kenya kupata mazao ya kuridhisha. Matatizo kama vile  haja ya kupanda mbegu zinazofaa kwa wakati unaofaa na mahali panapofaa na  kutumia mbolea inayofaa yanaweza kushughulikiwa kupitia kwa kilimo bora cha mimea na ufugaji. Hata hivyo, changamoto nyingine kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, mvua nyingi na kiangazi, mitetemeko ya ardhi, magonjwa, uharibifu, wadudu na mengine ni mambo ambayo mkulima hana uwezo juu yake.

Kwa nini uchukue bima ya mimea na mifugo?

Bima ya mifugo ni bima ya wanyama wa kufugwa kama vile ng’ombe, ndege (kuku, bata, batamzinga n.k), kondoo, mbuzi, nguruwe, farasi n.k. Wanyama hawa wanaweza kuathiriwa au kufa kutokana na kiangazi, magonjwa, ajali na misiba kama vile kuzuka kwa maradhi, wizi, moto, kupigwa na radi, kimbuga na mafuriko. Kwa upande mwingine, bima ya mazao ya mimea hushughulikia mazao ya vyakula kama vile ngano, shayiri, miwa, mahindi, mchele n.k. Bima ya mazao ya mimea na mifugo huwalipa wakulima kwa hasara dhidi ya mabadiliko katika mifugo na mazao ya mimea kutokana na hatari zilizotajwa hapo juu. Hii ni njia ya hakika ya kumfanya mkulima awe na ukakamavu kuimarisha shughuli zake baadaye.  

Jinsi bima ya mimea inavyofanya kazi

(1) Kampuni ya kutoa bima hukubaliana na mkulima kuhusu mazao yanayotarajiwa kwa kila ekari inayochukuliwa bima. Kiasi cha kuwekwa kwenye bima kitategemea jumla ya mazao katika eneo husika. Ikiwa wakati wa kuvuna mkulima anapata chini ya mazao yaliyotarajiwa  katika makubaliano, kampuni ya bima inalipia tofauti itakayopatikana hapo. Hivi, mkulima anahakikishiwa mavuno yake aliyotarajia licha ya kutofanikiwa kwa mimea;

(2) Mpango mwingine ni pale ambapo kampuni ya bima inamlinda mkulima dhidi ya hasara yoyote inayoweza kutukia kutokana na majanga kama vile  ukame, mafuriko, magonjwa, moto n.k. Mkulima anapaswa kupiga ripoti ya uharibifu kama huo kwa kampuni ya bima. Kampuni hiyo itakagua kiwango cha hasara na kupanga malipo ya kiasi cha hasara iliyopatikana kutokana na uharibifu huo.

Jinsi bima ya mifugo inavyofanya kazi

Mifugo ni pamoja na ng’ombe wa maziwa, ndege wa kufugwa, kondoo, mbuzi, nguruwe na farasi, miongoni mwa wengine. Bima ya mifugo hutolewa kwa  majanga kama vile magonjwa ya wanyama. Wakati mwingine, mkulima anaweza kulazimika kuchinja wanyama kwa misingi ya kiafya au kwa ushauri kutoka kwa daktari mtaalamu wa mifugo. Matatizo mengine ni pamoja na wizi, moto na kupigwa na radi. Bima inaweza kujumuisha vilevile kupotea kwa mifugo hao wanapokuwa wakisafirishwa.

Bima ya kilimo na mikopo kwa wakulima

Katika visa vingi, wakulima huhitaji mikopo kutoka taasisi za kifedha kununua vifaa vya kutumia shambani kama vile mbegu, mbolea na kemikali miongoni mwa vingine. Wakulima vilevile huhitaji pesa kununua kemikali, dawa, vifaa vya ujenzi n.k. Hata hivyo, taasisi za kifedha, haziwapi wakulima mikopo kwa urahisi bila udhamini. Wakiwa na bima, taasisi za kifedha hupata hakikisho kwamba mikopo hiyo italipiwa kukipatikana hasara mashambani. Mipangilio inaweza kufanywa ili malipo kwa hasara inayopatikana kutoka kwa bima ilipie mikopo waliyochukua wakulima kutoka kwa taasisi hizo za kifedha moja kwa moja.

Basi sasa nenda ukanunue bima ya mimea na mifugo ili ujihakikishie utulivu na amani wakati unapokuwa mgumu kwako.

Halmashauri ya Kudhibiti Bima (IRA)

IRA ilibuniwa na serikali mnamo mwaka wa 2006 kwa jukumu la kuweka maangalizi, kudhibiti sekta ya bima, kusimamia na pia kuhakikisha kwamba yeyote anayehusika na biashara za bima anatekeleza kazi yake kwa njia za usawa na pia kutilia maanani manufaa ya wanunuzi bima. Jukumu kuu la IRA ni kuwalinda wanunuzi wa bima na jamii kwa jumla. Nia ya IRA ni kuhakikisha kuwa wanunuzi hao wanapata huduma wanazolipia. IRA si kampuni ya bima  na hivyo haiuzi bima. IRA inawajibika kuhakikisha kuwa kampuni za bima zinashughulikia ipasavyo malalamishi yanayohusiana na bidhaa wanazouza. IRA huhakikisha kwamba ni malalamishi ya kweli pekee yanayoshughulikiwa bila kucheleweshwa. IRA pia inawajibika kuhakikisha kuwa wanunuzi bima wananunua kwenye kampuni zilizoidhinishwa na IRA wakiwemo maajenti na mabroka.

Huduma za IRA katika kusimamia maslahi ya Wakenya katika sekta ya bima ni za bila malipo. Unaweza kuelekeza suala lolote linalohusu bima kwa IRA ukitumia njia za mawasiliano zilizoorodheshwa nyuma ya brosha hii. 

S.L.P. 43505 – 00100 NAIROBI

Zep- Re Place Off Mara Road – Upper Hill, Nairobi

Simu:(254)- 020- 4996000, 0727 563110

Simu bila malipo – 0800724499

Kipepesi: (254)- 020 – 2710126

Baruapepe: commins@ira.go.ke

Tovuti: www.ira.go.ke

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *