Mahitaji na Manufaa ya bima

Halmashauri ya Kudhibiti Bima (IRA)

IRA ilibuniwa na serikali mnamo mwaka wa 2006 kwa jukumu la kuweka maangalizi, kudhibiti sekta ya bima, kusimamia na pia kuhakikisha kwamba yeyote anayehusika na biashara za bima anatekeleza kazi yake kwa njia za usawa na pia kutilia maanani manufaa ya wanunuzi bima. Jukumu kuu la IRA ni kuwalinda wanunuzi wa bima na jamii kwa jumla. Nia ya IRA ni kuhakikisha kuwa wanunuzi hao wanapata huduma wanazozilipia. IRA si kampuni ya bima  na hivyo haiuzi bima. IRA inawajibika kuhakikisha kuwa kampuni za bima zinashughulikia ipasavyo malalamishi yanayohusiana na bidhaa wanazouza. IRA huhakikisha kwamba ni malalamishi ya kweli pekee yanayoshughulikiwa bila kucheleweshwa. IRA pia inawajibika kuhakikisha kuwa wanunuzi bima wananunua kwenye kampuni zilizoidhinishwa na halmashauri hiyo wakiwemo maajenti na mabroka.

Huduma za IRA katika kusimamia maslahi ya Wakenya katika sekta ya bima ni za bila malipo. Unaweza kuelekeza suala lolote linalohusu bima kwa IRA ukitumia njia za mawasiliano zilizoorodheshwa nyuma ya brosha hii. 

Maana ya Bima

Bima ni njia moja ya kujikinga na matukio mbali mbali yanayotukumba maishani kila uchao. Bima ni mbinu mnununuzi bima hutumia ili kuhamishia kampuni ya bima mzigo wa hasara za kifedha. Ili apate kusimamiwa na kufidiwa na kampuni ya bima, mnunuzi sharti agharamie malipo ya bima ijulikanayo kwa Kiingereza  kama premium. Kisha, bima hulipa fidia kwa mnunuzi huyo anapohusika kwenya tukio bila kutarajia na kupata hasara za kifedha.

Jinsi Bima Inavyofanya kazi

Bima hufanya kazi katika msingi kwamba hasara na misiba hutukia mara kwa mara kwetu, kwa mali yetu au kwa jamii zetu. Bima huongozwa na busara kwamba ni vyema kujitayarisha mapema kwa tukio linaloweza kutokea bila kutarajiwa kuliko kungojea kuchukua hatua baada ya hasara kutokea.  Bima huongozwa na msingi kwamba ni wachache tu kati ya wanunuzi bima ambao hupata hasara. Kwa mfano, ni magari machache tu ambayo hupotea kila mwaka au ni nyumba chache tu huchomeka. Vilevile, ni watu wachache tu huwa wagonjwa au kuhusika kwenya ajali. Hata hivyo, hakuna anayejua ni nani atakayehusika kwenye hasara. Kwa hivyo, ni jambo la busara sana kwa wote walio katika hatari ya kufikwa na hasara kuamua kulipa ada (premium) ili kujitayarisha kwa tukio lolote.

Sababu ya kununua bima

Hakuna aliye na uhakika kuhusu kinachoweza kutokea maishani mwake wakati wowote. Waweza kuvamiwa na wezi nyumbani au katika biashara yako; moto waweza kuteketeza nyumba au viwanda; ajali zinazohusisha magari au pikipiki zinaweza kutokea kisha kusababisha majeraha, vifo au ulemavu. Mara nyingi visa kama hivi vinapotokea, wanaoathiriwa hujipata katika hali ya unyonge moyoni na umaskini kifedha. Hawawezi kukabiliana na athari zinazofuata. Kwa hivyo, hawa hulazimika kuita harambee au kukopa pesa kutoka kwa marafiki na jamaa zao. Huenda ikawa marafiki na jamaa hao pia wana mahitaji yao za kibinafsi. Mara nyingi, walioathirika hupaswa kuuza mali ya familia yenye thamani kubwa kama vile mashamba au mifugo kwa bei ya hasara. Madhumuni ya bima ni kuhakikisha kwamba pesa zitalipwa na kampuni za bima ili kusaidia kukabiliana na hasara.

Je, manufaa ya bima ni yapi?

Bima ni mbinu ya kukabiliana na changamoto zinazoathiri mali, maisha au afya ya binadamu. Mali ni chochote kinachothaminika na jamii kama maisha, mifugo, baiskeli, duka, mimea au nyumba miongoni mwa mengine. Kwa hivyo, kuchukua bima humwezesha mtu kupata manufaa yafuatayo:

  1. Kulipwa fidia kufuatia hasara

Bima husaidia pakubwa katika kulipa mali iliyopotea ama kuharibiwa. Kwa hivyo bima hulipa fidia na kumrejesha mhathirika katika hali alimokwa kifedha kabla ya tukio.  Hivyo basi, bima hunachangia sana kwa kuthibiti maendeleo ya jamii.

  • Kulinda familia

Bima ya maisha hulipa familia fidia kufuatia kifo au ulemavu kwa mwenye bima ambaye pia huenda akawa tegemeo la jamii.  Bima pia hulipa fidia ikiwa mwenye bima amefaulu kuishi hadi mwisho wa kipindi cha bima. Malipo haya hutegemea sana, kiwango au kiasi cha pesa mlioafikiana na kampuni ya bima mlipokamilisha mkataba huo. Hiki kiwango yajulikana kwa kiwango kama sums assured.

  • Utulivu na amani moyoni

Wale waliochukua bima kawaida huwa na utulivu na amani moyoni kwa ajili watakapopatikana na tukio lolote kama magonjwa au kuhusika katika ajali. Kampuni ya bima itagharamia athari zozote za kifedha zitakazotokea hadi kiwango walivyoafikiana. Hivyo, bima huwapa wateja ujasiri na kuondoa wasiwasi unaohusiana na misiba au hasara hizo za ghafla.

  • Kuweka akiba

Unaweza kuweka akiba kwa malipo kidogo kidogo kupitia bima ya maisha au malipo ya uzeeni (pension). Bima ya maisha ni mkataba wa kudumu ambao hulipia kiasi fulani cha pesa kipindi cha bima kitakapokamilika au mwenye bima kuaga dunia kabla ya kipindi kukamilika.  Ni jukumu la mnunuzi bima kuchagua kipindi cha bima. Njia kama hii huchochea mazoea ya watu kuwekeza kupitia bima kisha kutumia mapato ya akiba hii kwa siku zijazo ili kushughulikia mahitaji mbalimbali ya kifedha.

  • Udhamini wa kifedha

Bima ya maisha inaweza kutumiwa kama dhamana kwa mkopo kutoka kwa benki au kwa kampuni ya bima yenyewe. Pesa zinazokopwa huwa ni kima sawa na pesa za kusalimisha bimdhuru kukomaa kwa bima hiyo.

  • Faida kwa uwekezaji

Bima ya maisha husaidia wanunuzi kufikia malengo makuu maishani. Malengo haya ni pamoja na kununua au kujenga nyumba, kuelimisha watoto katika vyuo vya kati na vyuo vikuu na vilevile kujikimu kimaisha. Bima ya maisha inaweza kutumiwa kuweka pesa ili kuanzisha biashara siku zijazo.

Msamaha wa kodi

Serikali ya Kenya inakubali afueni ya kodi ya asilimia 15 kwa kila malipo ya bima (premium) hadi kiwango cha juu cha shilingi 5,000/=. Afueni hii hutolewa kwenye bima za maisha pekee. Hii ni njia moja ya Serikali ya Kenya kuwavutia watu wengi zaidi kununua bima ya maisha.

Halmashauri ya Kudhibiti Bima (IRA)

IRA ilibuniwa na serikali mnamo mwaka wa 2006 kwa jukumu la kuweka maangalizi, kudhibiti sekta ya bima, kusimamia na pia kuhakikisha kwamba yeyote anayehusika na biashara za bima anatekeleza kazi yake kwa njia za usawa na pia kutilia maanani manufaa ya wanunuzi bima. Jukumu kuu la IRA ni kuwalinda wanunuzi wa bima na jamii kwa jumla. Nia ya IRA ni kuhakikisha kuwa wanunuzi hao wanapata huduma wanazolipia. IRA si kampuni ya bima  na hivyo haiuzi bima. IRA inawajibika kuhakikisha kuwa kampuni za bima zinashughulikia ipasavyo malalamishi yanayohusiana na bidhaa wanazouza. IRA huhakikisha kwamba ni malalamishi ya kweli pekee yanayoshughulikiwa bila kucheleweshwa. IRA pia inawajibika kuhakikisha kuwa wanunuzi bima wananunua kwenye kampuni zilizoidhinishwa na IRA wakiwemo maajenti na mabroka.

Huduma za IRA katika kusimamia maslahi ya Wakenya katika sekta ya bima ni za bila malipo. Unaweza kuelekeza suala lolote linalohusu bima kwa IRA ukitumia njia za mawasiliano zilizoorodheshwa nyuma ya brosha hii. 

S.L.P. 43505 – 00100 NAIROBI

Zep- Re Place Off Mara Road – Upper Hill, Nairobi

Simu:(254)- 020- 4996000, 0727 563110

Simu bila malipo – 0800724499

Kipepesi: (254)- 020 – 2710126

Baruapepe: commins@ira.go.ke

Tovuti: www.ira.go.ke

Basi… sasa nenda ukachukue bima… kwa sababu maisha yako, familia yako na mali yako vyote ni muhimu!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *